============================
KAMPUNI
ya mawasiliano nchini ya Airtel imeahidi kuendelea kusaidia michezo mbalimbali
nchini ikiwa na lengo la kukuza maendeleo ya vijana.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana katika hafla fupi ya kukabidhi shilingi milioni tano
pamoja na fulana mia moja kama udhamini wa mbio za Rock City Marathon za mwaka
huu zenge kauli mbiu ‘tukuze utalii wa ndani kupitia michezo’, Afisa Uhusiano
wa Airtel, Bi Jane Matinde alisema kuwa kampuni yake itaendelea kusaidia
michezo mbalimbali nchini ikiwemo riadha ili kukuza maendeleo ya vijana.
“Udhamini
wetu wa shilingi milioni tano pamoja fulana mia moja katika mbio za Rock City
mwaka huu unalenga katika kusukuma maendeleo ya vijana kupitia michezo kwa
tunaamini kuwa michezo imekuwa ni chanzo kikubwa cha ajira duniani.
“Tunaahidi
kuendelea kusaidia michezo mingine kwa kuwa pia tunaamini kupitia michezo
mbalimbali tunaweza kutangaza vivutio vyetu vya utalii duniani. Mfano nzuri ni
mbio za mwaka huu za Rock City Marathon zitakazowakutanisha wanariadha
mbalimbali kutoka nchi jirani,” aliongeza Bi. Matinde.
Akipokea
hundi na fulana hizo, Mratibu wa mbio hizo kutoka katika kampuni ya Capital
Plus International (CPI), Bi. Grace Sanga aliishukuru kampuni ya Airtel kwa
kuendelea kusaidia mbio za Rock City na kuyahasa mashirikia na makampuni
mengine kuiga mfano wa kampuni hiyo.
“Tunaishukuru
Airtel kwa msaada wao kwa kuwa msaada huu utatusaidia tujiandae vizuri na Rock
City Marathon ya mwaka huu itakayofanyika Oktoba tarehe 28 katika uwanja wa CCM
Kirumba jijini Mwanza,” alisema Grace.
Grace
alisema kuwa mbali na Airtel wadhamini wengine ni pamoja na Shirika la Hifadhi
ya Jamii (NSSF), Parastal Pension Fund (PPF), Geita Gold Mine, African Barrick
Gold, Air Tanzania Company Ltd (ATCL), Mamlaka ya Taifa ya Mbuga za Wanyama
nchini (TANAPA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Nyanza Bottles, New Africa
Hotel na New Mwanza Hotel.
Aidha,
Bi Sanga aliwaasa wanariadha kujitokeza na kuanza kujisajili ili kushiriki
katika mbio hizo na kusema kuwa fomu za usajili zinapatikana katika ofisi za
uwanja wa CCM Kirumba, ofisi za kampuni ya Capital Plus International zilizopo
katika jengo la ATCL ghorofa ya tatu, ofisi za Bodi ya Utalii jengo la IPS
ghorofa ya tatu, Dar es Salaam, na zinapatikana katika tovuti ya www.rockcitymarathon.blogspot. com.
CPI
ilitangaza kuwa atakaeibuka kinara katika mbio za kilometa 21 mwaka huu kwa
wanaume na wanawake atazawadiwa shilingi milioni moja na laki mbili wakati
mshindi wa pili ataweka mfuko shilingi laki tisa na mshindi wa tatu ataondoka
na shilingi laki saba.