Promoting Domestic Tourism Through Sports.

Friday, September 14, 2012

Zawadi za Rock City Marathon 2012 zaboreshwa




Baadhi ya wawakilishi wa wadhamini wa mbio za Rock City Marathon 2012, wakifuatilia uzinduzi wa maandalizi ya mbiyo hizo ambazo zitafanyika katika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza Oktoba 28 mwaka huu. Uzinduzi huo ulifanyika katika hoteli ya New Africa Hotel Jijini Dar es Salaam mwezi uliopita.   
          ============================
WAANDAJI wa mbio za mwaka huu za Rock City Marathon, kampuni ya Capital Plus International (CPI) imetangaza maboresho ya zawadi zitakazoshindaniwa katika tamasha hilo litakalofanyika Oktoba 28 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Akitangaza zawadi hizo jijini Dar es Salaam jana, mratibu wa mbio hizo Grace Sanga alisema kuwa vinara wa mbio za kilometa 21 kwa upande wa wanaume na wanawake, watajishindia shilingi milioni moja na laki mbili, mshindi wa pili anaondoka na shilingi laki tisa na mshindi wa tatu atazawadiwa shilingi laki saba.
 “Maboresho ya zawadi yamefanyika katika mbio zote kutokana na kupata udhamini mzuri kutoka Shirika la Hifadhi la Taifa (NSSF), Airtel, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), African Barrick Gold, Nyanza Bottlers, Parastal Pensions Fund (PPF), Geita Gold Mine, TANAPA, Sahara Communications, ATCL, New Mwanza Hotel, na New Africa Hotel,” alisema Bi. Sanga.
Mbio za mwaka huu yenye kauli mbiu ‘tukuze utalii wa ndani kupitia michezo’ zitahusisha washiriki toka nchi jirani, ambao mbali na kushindana na wanariadha wa ndani, wanapata fursa ya kutembelea baadhi ya vivutio vya kitalii vinavyopatikana jijini Mwanza kama vile kisiwa cha Saannane, miamba inayocheza iliyopo Ukerewe pamoja na kuiona ziwa Victoria, hatua ambayo itasaidia kutangaza utalii wa Tanzania.
Alisema kuwa kwa washiriki watakaoshika nafasi kuanzia ya nne mpaka ya kumi, watazawadiwa shilingi laki moja na nusu, wakati wale watakaoshika nafasi kuanzia ya kumi na moja mpaka ishirini na tano watajipatia shilingi laki moja katika mbio za kilometa 21 kwa wote wanaume na wanawake.
 “Mbio nyinginezo zinazojumuisha washiriki wote, kama mbio za kilometa 5, vinara watajishindia shilingi elfu hamsini kila mmoja, mshindi wa pili atapata elfu thelathini na watatu ataondoka na shilingi elfu ishirini wakati watakaoangukia katika nafasi ya nne mpaka ishirini na tano wataondoka na elfu kumi na tano kila mmoja,” alisema Bi. Sanga.
Aliongeza kuwa kwa mbio za kilometa 3 zitakazo husisha wazee na walemavu, zawadi zitakuwa kama zifuatazo; Kinara atapata shilingi elfu hamsini, mshindi wa pili ataondoka na elfu thelathini na mshindi wa tatu ataweka mfukoni shilingi ishirini elfu wakati kwa watakaoshika nafasi ya nne mpaka ishirini na tano wataondoka na shilingi kumi na tano elfu kila mmoja.
Kwa mbio za kilometa 2 zitakazo husisha watoto kuanzia umri wa miaka saba mpaka kumi, mshindi ataondoka na shilingi thelathini elfu, wapili atapata shilingi ishirini elfu na watatu atapata shilingi elfu kumi na tano, wakati watakaoshika nafasi kuanzia ya nne mpaka ya ishirini na tano watajinyakulia shiringi elfu kumi kila mmoja.
Mwaka uliopita, vinara katika mbio za kilometa 21 walizawadiwa shilingi milioni moja kwa wanaume na wanawake, mshindi wa pili aliondoka na shilingi laki saba, wakati mshindi wa tatu aliondoka na shilingi laki tano.

Bofya hapa chini:-
Pakua fomu ya USAJILI - SWAHILI 
Dowload Registration Form - ENGLISH 

No comments:

Post a Comment