Promoting Domestic Tourism Through Sports.

Thursday, September 20, 2012

AIRTEL yaahidi kuendelea kusaidia maendeleo ya michezo nchini



Afisa Uhusiano wa kampuni ya Airtel Tanzania Bi Jane Matinde (kulia) akimkabidhi hundi ya shilingi milioni tano Meneja Matukio wa kampuni ya Capital Plus International ambaye pia ni Mratibu wa mbio za Rock City Marathon za mwaka huu Bi Grace Sanga jijini Dar es Salaam jana kama sehemu udhamini wa mbio hizo zitakazofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza tarehe 28 Oktoba. Airtel pia walikabidhi fulana mia nne zitakazotumika katika mbio hizo. 
Afisa Uhusiano wa kampuni ya Airtel Tanzania Bi Jane Matinde (kulia) akimkabidhi moja kati ya T-sheti mia nne Meneja Matukio wa kampuni ya Capital Plus International ambaye pia ni Mratibu wa mbio za Rock City Marathon za mwaka huu Bi Grace Sanga jijini Dar es Salaam jana kama sehemu udhamini wa mbio hizo zitakazofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza tarehe 28 Oktoba. Airtel walikabidhi T-sheti mia nne pamoja na milioni tano kusaidia mbio hizo.
                             ============================

KAMPUNI ya mawasiliano nchini ya Airtel imeahidi kuendelea kusaidia michezo mbalimbali nchini ikiwa na lengo la kukuza maendeleo ya vijana.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika hafla fupi ya kukabidhi shilingi milioni tano pamoja na fulana mia moja kama udhamini wa mbio za Rock City Marathon za mwaka huu zenge kauli mbiu ‘tukuze utalii wa ndani kupitia michezo’, Afisa Uhusiano wa Airtel, Bi Jane Matinde alisema kuwa kampuni yake itaendelea kusaidia michezo mbalimbali nchini ikiwemo riadha ili kukuza maendeleo ya vijana.
“Udhamini wetu wa shilingi milioni tano pamoja fulana mia moja katika mbio za Rock City mwaka huu unalenga katika kusukuma maendeleo ya vijana kupitia michezo kwa tunaamini kuwa michezo imekuwa ni chanzo kikubwa cha ajira duniani.
“Tunaahidi kuendelea kusaidia michezo mingine kwa kuwa pia tunaamini kupitia michezo mbalimbali tunaweza kutangaza vivutio vyetu vya utalii duniani. Mfano nzuri ni mbio za mwaka huu za Rock City Marathon zitakazowakutanisha wanariadha mbalimbali kutoka nchi jirani,” aliongeza Bi. Matinde.
Akipokea hundi na fulana hizo, Mratibu wa mbio hizo kutoka katika kampuni ya Capital Plus International (CPI), Bi. Grace Sanga aliishukuru kampuni ya Airtel kwa kuendelea kusaidia mbio za Rock City na kuyahasa mashirikia na makampuni mengine kuiga mfano wa kampuni hiyo.
“Tunaishukuru Airtel kwa msaada wao kwa kuwa msaada huu utatusaidia tujiandae vizuri na Rock City Marathon ya mwaka huu itakayofanyika Oktoba tarehe 28 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza,” alisema Grace.
Grace alisema kuwa mbali na Airtel wadhamini wengine ni pamoja na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Parastal Pension Fund (PPF), Geita Gold Mine, African Barrick Gold, Air Tanzania Company Ltd (ATCL), Mamlaka ya Taifa ya Mbuga za Wanyama nchini (TANAPA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Nyanza Bottles, New Africa Hotel na New Mwanza Hotel.
Aidha, Bi Sanga aliwaasa wanariadha kujitokeza na kuanza kujisajili ili kushiriki katika mbio hizo na kusema kuwa fomu za usajili zinapatikana katika ofisi za uwanja wa CCM Kirumba, ofisi za kampuni ya Capital Plus International zilizopo katika jengo la ATCL ghorofa ya tatu, ofisi za Bodi ya Utalii jengo la IPS ghorofa ya tatu, Dar es Salaam, na zinapatikana katika tovuti ya www.rockcitymarathon.blogspot.com.
CPI ilitangaza kuwa atakaeibuka kinara katika mbio za kilometa 21 mwaka huu kwa wanaume na wanawake atazawadiwa shilingi milioni moja na laki mbili wakati mshindi wa pili ataweka mfuko shilingi laki tisa na mshindi wa tatu ataondoka na shilingi laki saba. 

Bofya hapa chini:-


Friday, September 14, 2012

Zawadi za Rock City Marathon 2012 zaboreshwa




Baadhi ya wawakilishi wa wadhamini wa mbio za Rock City Marathon 2012, wakifuatilia uzinduzi wa maandalizi ya mbiyo hizo ambazo zitafanyika katika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza Oktoba 28 mwaka huu. Uzinduzi huo ulifanyika katika hoteli ya New Africa Hotel Jijini Dar es Salaam mwezi uliopita.   
          ============================
WAANDAJI wa mbio za mwaka huu za Rock City Marathon, kampuni ya Capital Plus International (CPI) imetangaza maboresho ya zawadi zitakazoshindaniwa katika tamasha hilo litakalofanyika Oktoba 28 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Akitangaza zawadi hizo jijini Dar es Salaam jana, mratibu wa mbio hizo Grace Sanga alisema kuwa vinara wa mbio za kilometa 21 kwa upande wa wanaume na wanawake, watajishindia shilingi milioni moja na laki mbili, mshindi wa pili anaondoka na shilingi laki tisa na mshindi wa tatu atazawadiwa shilingi laki saba.
 “Maboresho ya zawadi yamefanyika katika mbio zote kutokana na kupata udhamini mzuri kutoka Shirika la Hifadhi la Taifa (NSSF), Airtel, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), African Barrick Gold, Nyanza Bottlers, Parastal Pensions Fund (PPF), Geita Gold Mine, TANAPA, Sahara Communications, ATCL, New Mwanza Hotel, na New Africa Hotel,” alisema Bi. Sanga.
Mbio za mwaka huu yenye kauli mbiu ‘tukuze utalii wa ndani kupitia michezo’ zitahusisha washiriki toka nchi jirani, ambao mbali na kushindana na wanariadha wa ndani, wanapata fursa ya kutembelea baadhi ya vivutio vya kitalii vinavyopatikana jijini Mwanza kama vile kisiwa cha Saannane, miamba inayocheza iliyopo Ukerewe pamoja na kuiona ziwa Victoria, hatua ambayo itasaidia kutangaza utalii wa Tanzania.
Alisema kuwa kwa washiriki watakaoshika nafasi kuanzia ya nne mpaka ya kumi, watazawadiwa shilingi laki moja na nusu, wakati wale watakaoshika nafasi kuanzia ya kumi na moja mpaka ishirini na tano watajipatia shilingi laki moja katika mbio za kilometa 21 kwa wote wanaume na wanawake.
 “Mbio nyinginezo zinazojumuisha washiriki wote, kama mbio za kilometa 5, vinara watajishindia shilingi elfu hamsini kila mmoja, mshindi wa pili atapata elfu thelathini na watatu ataondoka na shilingi elfu ishirini wakati watakaoangukia katika nafasi ya nne mpaka ishirini na tano wataondoka na elfu kumi na tano kila mmoja,” alisema Bi. Sanga.
Aliongeza kuwa kwa mbio za kilometa 3 zitakazo husisha wazee na walemavu, zawadi zitakuwa kama zifuatazo; Kinara atapata shilingi elfu hamsini, mshindi wa pili ataondoka na elfu thelathini na mshindi wa tatu ataweka mfukoni shilingi ishirini elfu wakati kwa watakaoshika nafasi ya nne mpaka ishirini na tano wataondoka na shilingi kumi na tano elfu kila mmoja.
Kwa mbio za kilometa 2 zitakazo husisha watoto kuanzia umri wa miaka saba mpaka kumi, mshindi ataondoka na shilingi thelathini elfu, wapili atapata shilingi ishirini elfu na watatu atapata shilingi elfu kumi na tano, wakati watakaoshika nafasi kuanzia ya nne mpaka ya ishirini na tano watajinyakulia shiringi elfu kumi kila mmoja.
Mwaka uliopita, vinara katika mbio za kilometa 21 walizawadiwa shilingi milioni moja kwa wanaume na wanawake, mshindi wa pili aliondoka na shilingi laki saba, wakati mshindi wa tatu aliondoka na shilingi laki tano.

Bofya hapa chini:-
Pakua fomu ya USAJILI - SWAHILI 
Dowload Registration Form - ENGLISH