Promoting Domestic Tourism Through Sports.

Saturday, October 27, 2012

Usajili wa mbio za Rock City 2012 wasogezwa mbele

Baadhi ya wanariadha wakishiriki katika mbio za Rock City (Picha kutoka Maktaba)
WAANDAJI wa mbio za Rock City Marathon 2012 wametangaza kusogeza mbele usajili wa kushiriki mbio hizo mpaka Oktoba 26 ili kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kushiriki katika mbio hizo. 
Akizungumza na waandishi jijini Dar es Salaam jana, mratibu wa mbio hizo toka kampuni ya Capital Plus International (CPI), alisema kuwa wameamua kusogeza mbele usajili kutokana na namba ya waombaji kuendelea kuongezeka ili kushiriki mbio za mwaka huu.
Bi Sanga alisema tukio hilo linaloandaliwa na kampuni ya Capital Plus International (CPI) na kudhaminiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Taifa ya Jamii (NSSF), Airtel Tanzania, Geita Gold Mine, Shirika la Ndege la Air Tanzania, Parastal Pension Fund (PPF), African Barrick Gold, New Africa Hotel, Nyanza Bottles, New Mwanza Hotel, TANAPA na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) limewavutia washiriki wengi kutoka nchi mbalimbali ambao wasingependa kukosa mbio hizo mwaka huu.
“Tumekuwa tukipokea simu kutoka kwa washiriki mbalimbali, kutoka Chama cha Riadha nchini na kutoka nchi jirani ambao wanataka kupewa nafasi ya kushiriki katika mbio za mwaka huu. Sisi kama waandaji tumeona ni vyema tuwapatia nafasi ya kujisajili kwa kuwa ushiriki wa utasadia lengo la mbio za mwaka huu lifikiwe la kutangaza utalii kupitia michezo,” alisema Sanga.
Bi Sanga aliongeza kuwa washiriki na washabiki wa mbio za Rock City za mwaka huu watapata fursa ya kumshuhudia msanii maarufu wa Tanzania Juma Nature a.k.a Sir Nature na kundi lake la TMK Wanaume wakitumbuiza wakati wa mbio hizo.   
Alisema kuwa washiriki kutoka nchi tisa wameshathibitisha kushiriki mbio za kilometa 21 za mwaka huu zitakazofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwaka tarehe 28 mwezi Oktoba.
Bi Sanga alisema kuwa mialiko katika mbio hizo imeongezwa na wanariadha kutoka Afrika Mashariki na nchi nyingine za ulaya wanatarajiwa kushiriki. Akilitaja nchi hizo kuwa ni Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Demokrasia ya Watu wa Kongo (DRC) na nchi nyingine za ulaya kama Australia, India, Canada na Marekani.
Alisema kuwa wanauhakika mkubwa kuwa namba ya washiriki mwaka huu itaongezeka mara dufu kutokana na uboreshwaji wa zawadi.
“Tunatarajia kuwa na washiriki wengi zaidi toka nchi za nje ukilinganisha na miaka iliyopita. Hii inaonyesha kukua mbio hizi na kuwa ushindani wa mbio za mwaka utakuwa mkali zaidi,” alisema Bi Sanga.
Mbio hizo za kila mwaka zimegawanyishwa katika makundi matano, ambapo kutakuwa na mbio za kilomita 21 kwa wanawake na wanaume, kilomita tano kwa watu wote, kilomita tatu kwa watu wenye ulemavu, kilomita tatu kwa wazee (miaka 55 na kuendelea) na kilomita mbili kwa watoto umri kati ya miaka saba mpaka kumi. 
Bi. Sanga alisema kuwa mbio hizo zinazoonyesha mafanikio makubwa toka zizinduliwe mwaka 2009, zinalenga kukuza utalii wa ndani kupitia michezo kama kauli mbiu yake inavyosema ‘tukuze utalii wa ndani kupitia michezo’.
“Jiji la Mwanza ni tajiri sana katika vivutio vya utalii na tumelenga kumpitia mbio hizi kuvitangaza vivutio hivyo. Mbio za kilomita 21 zitaanza katika uwanja wa CCM Kirumba na kupita njia tofauti tofauti na kurudi CCM Kirumba”, alisema.
Alisema pia pesa itakayopatikana ikitokana na ada ya usajili toka kwa washiriki moja kwa moja itapelekwa katika mfuko wa msaada kwa watu wenye ulemavu waishio jijini Mwanza.  
Fomu za usajili za mbio hizo zinapatikana katika uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza, Ofisi za Kampuni ya Capital Plus International Ltd zilizopo jengo la ATC ghorofa ya tatu, na pia zinapatikana katika blog ya rockcitymarathon.blogspot.com.
 


No comments:

Post a Comment